Uendelezaji mifumo ya masoko kuleta mapinduzi kwenye sekta kubwa zaidi ya uchumi Tanzania

Uendelezaji mifumo ya masoko kuleta mapinduzi kwenye sekta kubwa zaidi ya uchumi Tanzania

Mahojiano na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Agricultural Markets Development Trust (AMDT)

Swali: Lini AMDT ilianzishwa na jukumu lake kubwa ni lipi?

Jibu: Taasisi ya Agricultural Markets Development Trust (AMDT) ilianzishwa mwaka 2014 kufuatia majadiliano ya wadau kuamua njia na mkakati muafaka wa kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya kilimo. Baada ya hapo tulipata usajili rasmi mwaka 2015. Maono yetu makuu ni kuwezesha maendeleo endelevu katika jamii yetu kupitia sekta mama ya kilimo.

Jukumu kubwa la AMDT ni kuwezesha na kuboresha mabadiliko makubwa ya kimkakati kwenye mifumo ya masoko ya sekta za kilimo. Hii ni kwa kutambua kuwa kilimo ndio msingi wa ustawi wa jamii nyingi maskini na wale wanaojitahidi kujikwamua nchini. Kimsingi, uwezeshaji huu kwenye kilimo unalenga kufungua vizingiti vilivyopo kwenye mifumo ya masoko vinavyotatiza ushiriki mpana na mafanikio kwa wakulima, haswa wadogo. Lengo kuu ni kutafsiri mafanikio haya kwa ongezeko halisi la kipato na fursa za ajira.

Swali: Kulikua na umuhimu gani kuanzisha AMDT? 

Jibu: Matamanio ya Tanzania kuwa Taifa la Uchumi wa Kati yanabebwa zaidi na tija na ukuaji wa sekta ya kilimo. Kwa mantiki hiyo basi, sababu ya msingi ya kuanzishwa AMDT ni kuchangia katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kuwezesha kuongezeka kwa kipato kwa wakulima wengi walio wadogo na pia kufungua fursa za ajira katika ngazi zote za minyororo ya thamani ya sekta zetu za kilimo.

Swali: Ni kivipi AMDT hutekeleza jukumu lake? 

Jibu: Kimsingi, AMDT ni muwezeshaji zaidi badala ya mtekelezaji wa moja kwa moja. Kazi yake kubwa ni kuwezesha uboreshaji wa mazingira yanayorahisisha na kuhamasisha mashirikiano baina ya washiriki na biashara ndani ya sekta ya umma na sekta ya binafsi katika kutatua changamoto kuu katika sekta za kilimo. Kufanya hivi tunaongeza juhudi za pamoja za ujenzi na uwekezaji katika sekta hizo. Kwa kukumbushia tu, AMDT kimsingi ilianzishwa kama chombo maalum kushughulikia changamoto za kimkakati ambazo mashirika na wadau wengi wa maendeleo walishindwa kupata utatuzi endelevu kwenye kilimo. Kwa hivyo kwa kifupi, AMDT ipo hapa kuchagiza na kuchochea mifumo ya masoko yenye tija na inayofungua fursa kwa wakulima wadogo pamoja na wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs) katika minyororo ya thamani ya mazao tunayowezesha.

Swali: Ni zipi sekta na vipaumbele vya AMDT katika shughuli zake? 

Jibu: Kiufundi, minyororo ya thamani kwetu sisi ni milango tu ya kuingilia kwenye sekta tunazowezesha. Na humo ndani ya sekta tuna malengo yetu na utaratibu wa kuyafikia. Haya ni pamoja na utatuzi wa changamoto za kimfumo. Msingi wake haswa ni kuhakikisha kwamba juhudi zetu zinafaidisha watu, haswa wale nguvukazi toka jamii maskini, kutokana na utekelezaji wa shughuli na miradi yetu.

Kwa sasa tunashughulikia sekta kuu tatu za alizeti, mahindi na jamii ya mikunde. Katika sekta hizi tunashughulika na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara mfano kuwezesha maboresho ya sera na kupaza sauti za wadau wakuu katika sekta. Na katika miradi na jitihada zetu zote, ushirikishwaji wa wanawake na vijana ni jambo la kimkakati, mtambuka na la lazima katika ngazi zote.

Swali: Nini tofauti kati ya falsafa yenu ya uendelezaji wa mifumo ya masoko ikilenga jamii maskini na ile ya uboreshaji wa minyororo ya thamani kwenye kilimo? 

Jibu: Kwa kifupi sana falsafa, mbinu au metholojia yetu ya uendelezaji mifumo ya masoko inaenda ndani zaidi ya kuboresha minyororo ya thamani na wadau wake. Hii inalenga kufungua fursa na njia za tija na mafanikio kwa wahusika wa sekta, tukilenga zaidi jamii maskini kushiriki kikamilifu kwenye mifumo ya masoko. Falsafa hii kwa mapana yake inalenga matokeo endelevu yanayogusa watu. Hiyo ndio metholojia yetu.

Sasa kwa upande wake, uboreshaji minyororo ya thamani kwenye kilimo inalenga zaidi kuongeza thamani kwa bidhaa katika sekta husika kwa mara nyingi bila kuwa na msisitizo wa kufaidisha au kugusa maisha ya jamii maskini kule chini, ambao ndio nguvukazi kubwa kwenye kilimo. Na pia njia hii hailengi matokeo makubwa na ya muda mrefu. Inalenga sekta husika zaidi.

Swali: Kwa Tanzania ya leo hii, ni vipi mnaweza kuhamasisha jamii za vijijini kujikita kwenye kilimo, badala ya kukimbilia mijini na kufanya kazi za ufundi na maofisini? 

Jibu: Nadhani njia bora zaidi ya kuwavutia watu maskini kujikita kwenye kilimo ni kwa kutatua changamoto na matatizo yote yanayoathiri shughuli na biashara zao za kilimo. Hizo ndio zinazuia kipato chao. Mfano ukishashughulikia tatizo la upatikanaji kirahisi na kwa bei inayohimilika pembejeo za kilimo, au huduma muhimu kama fedha na mitaji, kisha ukahakikisha kuna soko la uhakika kwa mazao na bidhaa za kilimo chao, utakifanya kilimo kuwa shughuli inayokimbiliwa na wengi zaidi. Na falsafa yetu inaangalia sekta mama ya kilimo nchini katika maono hayo.

Swali: Ni zipi hasa huduma zenu kwenye mikoa mnayotekeleza miradi? Na zinatolewaje kwa walengwa? 

Jibu: AMDT haitekelezi moja kwa moja miradi bali tunafanya kazi kupitia wadau na wabia wetu waliopo kwenye mifumo ya masoko ya sekta husika. Kwa hiyo huduma zetu na shughuli zetu zinategemea zaidi changamoto na matatizo yaliyopo kwenye mfumo husika wa masoko. Utatuzi wake huweka mazingira bora zaidi kwa wazalishaji wadogo maskini katika sekta za kilimo kufaidika zaidi.

Kwa mfano chukulia changamoto ya upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha ili wakulima wadogo wapate mikopo, bima nk. Humo tunafanya kazi na wabia na wadau wa sekta binafsi waliopo kwenye mifumo hiyo ya fedha. Na vilevile kwenye masuala ya uchakataji mazao ya kilimo, utafutaji masoko, teknolojia na mashine muhimu kwenye kilimo nk.

Swali: Ni miradi ipi mingine mnaitekeleza kwa sasa? Na mipango ya baadae ipo vipi? 

Jibu: Kwa sasa tunawezesha miradi katika mikoa saba kupitia wadau wetu katika mifumo ya masoko huko. Mikoa hii ni Ruvuma, Mbeya, Iringa, Rukwa, Dodoma, Singida na Manyara. Tunawezesha miradi miwili (2) katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mahindi, mitano (5) kwenye alizeti na mitatu (3) kwenye jamii ya mikunde.

Pia tuna miradi ya kimkakati tunatekeleza kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo inayolenga kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora kwenye alizeti, ambapo tunafanya kazi na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ya Ilonga. Vilevile tunashirikiana na Wizara kwenye kujenga uwezo na weledi kwa Maafisa Ugani wa umma na upatikanaji wa huduma zao sehemu mbalimbali nchini. Mradi huu wa kimkakati ni wa mafunzo rejea na tunafanya kazi na Idara ya Mafunzo na Ugani na Utafiti pale wizarani.

Miradi yetu ya baadae itategemea tathmini kubwa ya matokeo ya uwezeshaji wetu katika kipindi hiki. Tathmini hii itafuata viwango vya kimataifa vya DCED (Donor Committee for Enterprise Development). Tathmini itatuonyesha miradi yenye mafanikio makubwa ambayo tunaweza kuwekeza zaidi ili kufikia watu wengi katika maeneo mengine mapya. Pia itatupa picha ya maeneo ambayo yatakua yamekua na kuchanua na hivyo kutohitaji uwezeshaji wetu. Lakini pia, pengine muhimu zaidi ni mahitaji yetu kama nchi katika kipindi kijacho yatakua na nafasi kwetu katika kupanga miradi ipi tuweke jitihada na kipaumbele kwetu.

Swali: Ni changamoto zipi kubwa mnakabiliana nazo katika uwezeshaji kwenye kilimo na mnakabiliana vipi nazo? 

Jibu: Kwa sasa changamoto kubwa ni kwamba tunakamilisha kipindi cha awamu kwanza (Phase 1) cha programu yetu mwezi Juni 2022. Kwa hiyo kwa sasa tunashughulika zaidi katika kutafuta rasilimali kwa ajili ya awamu ya pili (Phase 2). Tayari menejimenti yetu, Bodi pamoja na vyombo vya juu vya maamuzi wanatengeneza mkakati katika hili. Kuna uwakilishi wa Serikali katika ngazi hii. Na katika ngazi ya sekretarieti, bado tunatathmini na kuboresha mifumo na taratibu zetu ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi zetu na kufaidisha Taifa zaidi.

Swali: Mnapataje rasilimali fedha kwa ajili ya programu yenu?

Jibu: AMDT ilianzishwa kama Mfuko Maalum na serikali za Denmark, Switzerland, Ireland na Sweden kwa makubaliano na Tanzania. Awamu ya Kwanza (Phase 1) ya utekelezaji wa programu hii kinakamilika mwezi Juni mwakani. Kwa hivyo jitihada zetu zipo katika kukaribisha na kuvutia wadau na wabia wengine kwa ajili ya kuwekeza kwenye awamu ya pili itakayoanza Julai 2022 mpaka Julai 2027.

Swali: Nini mafanikio yenu makubwa kwa kipindi hiki cha kwanza? 

Jibu: Tunajivunia kuwa mdau wa kimkakati katika sekta ya kilimo hapa Tanzania. Tunajivunia pia; kwanza – kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti kwa kushirikiana na wabia na wadau wetu kama Quality Food Products Ltd, Bitrade, Silverland na Sunflower Development Company (SDC). Baadhi ya mbegu hizi zimekua maarufu sana nchini, mfano Hysun 33, high Oleic (Anciella) na Agwara 4. Zinapatikana nchi nzima kwa sasa; pili, tumewezesha na kuhamasisha kilimo cha mkataba kati ya wachakataji na wakulima wadogo katika minyororo ya thamani ya alizeti, mahindi na mikunde/maharage; tatu, tumewezesha na kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika maeneo muhimu sana ya kimkakati kwenye kilimo ikiwemo uwezeshaji mkubwa kwa taasisi ya serikali ya TARI Ilonga katika uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za alizeti kwa kuwashirikisha makampuni ya Kitanzania. Pia tumewezesha na tunashirikiana na Wizara katika kuboresha huduma za ugani kwenye kilimo nchini. Mradi huu unahusisha mafunzo kwa Maafisa Ugani 1,340 wa serikali katika halmashauri 46 za wilaya kwenye mikoa 14 nchini.

Related Posts
Leave a Reply

Your email address will not be published.Required fields are marked *